Kuhusu Soma Biblia

Soma Biblia ni tawi la kazi ya misheni ya kimataifa ya Danish Lutheran Mission Tanzania. Lengo la Soma Biblia ni kwamba Biblia na vitabu vingine vya Kikristo vipatikane kwa wengi iwezekanavyo, kwa mfano kwa kuanzisha maduka ya vitabu sehemu mbalimbali nchini. Mwaka 2007 Soma Biblia ilikuwa imekuwepo Tanzania miaka 20, lakini hata katikati ya mwongo wa 1980, Bw. Fritz Larsen, mmisionari maeneo ya Sumbawanga, aliwaza kuanzisha kazi ya fasisi yenye kujitegemea. Kipindi kile fasihi ya Kikristo ilipatikana kwa sehemu, lakini watu wachache walifaidi, kutokana na watoaji wa vitabu kukosa njia za kuvisambaza. Huu ulikuwa mwanzo wa Soma Biblia, ambayo kwa miaka 5 ya kwanza ilihusika tu na usambazaji wa fasihi ya Kikristo Tanzania ikiwa na makao makuu Iringa. Kipindi kile tayari ilionekana kwamba jambo la kipaumbele liwe kazi ile ya kufikisha vitabu mikoani, na hadi sasa ni dhana ongozi. Mmisionari Erik Nielsen, aliyewasili Iringa 1987, alikuwa mwajiriwa wa kwanza katika kazi ya fasihi ya DLM Tanzania. Akiwa Iringa, alijaza gari lake Biblia na vitabu vya Kikristo, akaenda Dar es Salaam kuwauzia wauzaji hapo, ndipo akanunua vitabu vipya kwao akajaza tena gari lake akaendelea na safari kwenda kaskazini Moshi na Arusha akawauzia wauzaji hapo n.k. Uboreshaji huo wa usambazaji wa Biblia, ulisababisha Chama cha Biblia Tanzania kuongeza uzalishaji wao, na kwa njia hiyo Biblia ilianza kupatikana kwa watu wengi zaidi.

Biblereader.www

Mwaka 1992 Danish Lutheran Mission ilipata idara ya uchapishaji iliyosajiliwa kwa jina la Soma Biblia. Idara hiyo inatafsiri vitabu pamoja na kuchapisha vitabu vipya kwa Kiswahili. Na pia imeanzisha Shule ya kujifunza Biblia kwa njia ya Posta. Soma Biblia ina vituo 3 Tanzania. Cha kwanza kilianzishwa Iringa mwaka 1987 na duka jipya pamoja na nyumba kwa msimamizi wa kazi viliwekwa wakfu mwaka 1989. Mwaka 1998 nyumba ilinunuliwa Dar es Salaam na duka likafunguliwa hapo. Tena mwaka 2005 nyumba nyingine ikakodiwa Mwanza ambapo sehemu ya nyumba inatumika kama duka. Magari yaliyojaa vitabu yanatoka katika vituo hivyo vyote ili kusambaza vitabu kwa wauzaji wengine, kuviuza barabarani au katika masoko ama vitabu vinauzwa makanisani Jumapili baada ya ibada.

somabiblia.www

Kwa sababu ya huduma hiyo idadi ya maduka ya vitabu imeongezeka Tanzania, nayo imerahisisha upatikanaji wa Biblia na vitabu vinginge vya Kikristo kwa watu wengi Tanzania. Soma Biblia ni huduma inayojitegemea, nayo haiko chini ya dhehebu fulani, ingawa Soma Biblia inashirikiana kwa karibu na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri na Kanisa la Moravian. Si lengo la Soma Biblia kuanzisha makanisa wala sharika.