Riziki 2/2026 - Mavuno ni mengi Watenda kazi wachache
Cathbert Msemo
Je, ni nani atakayejitokeza katika shamba la Bwana?
“Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache” (Mt 9:37). Maneno haya ya Yesu yanatufanya tusimame na kutafakari hali halisi ya dunia yetu leo. Watu wengi wanahitaji kusikia Injili, kupata faraja na kuonja upendo wa Mungu, lakini idadi ya wale wanaojitoa kwa moyo kufanya kazi ya umisioni ni ndogo. Mara nyingi tunakaa kimya kana kwamba jukumu hili ni la wachache tu, ilhali Bwana anatuita sisi sote.
Katika toleo hili, tunakumbushwa kwamba kila muumini wa Yesu ana nafasi yake katika shamba la Bwana. Hakuna aliye mdogo mno au kuweza kutoa udhuru mwingine kwamba hana nafasi ya kushiriki. Kuna nafasi kwa kila huduma ndogo na tendo la upendo. Kipekee Yesu anatuambia kuwa tumwombe yeye, Bwana wa mavuno, apeleke watendakazi katika mavuno yake.
Swali la msingi ni: Je, mavuno hayo ya Bwana Yesu yana maana gani kwangu? Je, wito wake unanifanya kuchangia kwa sala yangu ndogo, tendo langu la upendo, au huduma yangu katika Kanisa lake?
Wito wa Yesu si kwa jumuiya pekee bali wa binafsi kwa moyo wangu na moyo wako. Je, niko tayari kuhesabiwa miongoni mwa wale wachache wanaojitolea? Je, nitajitokeza na kusema: “Niko hapa, nitume mimi”?
Mavuno yakiwa ya waumini wote, ni dhahiri kuwa kila mmoja ana nafasi ya kushiriki. Ni mwaliko wa kujiandaa na kujitolea kwa kuonesha upendo wa Kristo kwa vitendo. Katika toleo hili, tunahimizwa tusisubiri wengine wafanye, bali tuwe tayari kushiriki katika kuleta mavuno kwa ajili ya ufalme wa Mungu.