Soma Biblia ni nani?
Shirika la Kikristo hapa Tanzania
Mchapishaji na msambazaji wa maandiko ya Kikristo
Taasisi ya hisani isiyo ya kifaida wala ya kisiasa
Tunalenga kuwafikishia watu wa rika zote Injili ya Yesu Kristo
Tunaamini kwamba
Biblia ni Neno la Mungu, lisilo na makosa katika mafundisho yake, la kuaminika katika kila linachosema, na linatosha kabisa kuwa msingi wa imani na maisha ya Mkristo.
Ungamo la Imani la Kilutheri ni tafsiri sahihi na muhtasari wa kweli wa ujumbe wa Biblia.
Maono Yetu
Neno la Injili kwa Rika Zote Tanzania!
Dhamira Yetu
Kueneza Neno la Injili kwa rika zote Tanzania kupitia uandishi, uchapishaji, uuzaji na usambazaji wa Biblia na machapisho ya Kikristo yenye mafundisho ya Biblia. Kwa kufanya hivyo, tunaliwezesha Kanisa kuwafundisha Wakristo wa rika zote Neno la Mungu kwa ajili ya imani na maisha yao, na kuwaandaa kuwafikia wale ambao bado hawajaisikia Injili.
Tunachofanya
Kwa sasa, Soma Biblia ina maduka saba (8) ya vitabu nchini Tanzania yaliyopo Dar es Salaam (Mikocheni B na Mbezi Luis), Arusha, Mwanza, Mbeya, Dodoma, Iringa na Makambako.
Kila wakati, watumishi husafiri katika maeneo mbalimbali ya Tanzania wakiwa na magari yaliyobeba Biblia na vitabu vya Kikristo. Lengo letu ni kuhakikisha kwamba hata watu wanaoishi katika maeneo ya mbali kabisa wanapata fursa ya kupata Biblia na machapisho ya Kikristo yanayozingatia mafundisho ya Biblia.
Kupitia idara yetu ya uchapishaji, tunachapisha vitabu, vijitabu vya Injili, kalenda, pamoja na majarida mawili yanayotolewa mara nne kwa mwaka:
RIZIKI – kwa watumishi wa Kanisa.
TWENDE – kwa watoto.
Pia tunaendesha kozi za kujifunza kwa njia ya mtandao kwa wale wanaotamani kujifunza kwa kina mafundisho mbalimbali ya Kikristo kupitia vitabu vyetu. Aidha, tunawasaidia waandishi Wakristo wa Kitanzania kuendeleza uwezo wao wa uandishi ili kukidhi hitaji la machapisho ya Kikristo yanayotegemea mafundisho ya Biblia kwa lugha ya Kiswahili.
Historia Yetu kwa Ufupi
Shirika la Soma Biblia lilianzishwa tarehe 1 Januari 2015 baada ya kuunganishwa kwa huduma mbili za uchapishaji wa maandiko ya Kikristo zilizokuwa zikihudumu nchini Tanzania kwa takribani miaka 30 iliyopita. Huduma hizo ni:
Soma Biblia, iliyokuwa ikiendeshwa na Danish Lutheran Mission.
Scripture Mission, iliyokuwa ikiendeshwa kwa ushirikiano wa Scripture Mission East Africa na Norwegian Lutheran Mission.
Makao makuu ya Soma Biblia yako katika eneo la Danish Lutheran Mission, Mikocheni B, Dar es Salaam. Idara ya uchapishaji ina ofisi zake katika eneo la Scripture Mission, Arusha.
Soma Biblia management:
Rev. Phares Kakulima, PhD (Director), Bwigane Mwamasange (Finance Manager), Philip Bach-Svendsen (Publishing Manager), Mathayo K. Massawe (Sales Manager)
Soma Biblia board:
Ole Malmgaard (Chair person), David Ngassapa, Godwin Kimaro