Ufalme wa Mungu unaonekana katika haki


Haki ni nini? Je, haki huamuliwa na sheria za wanadamu au na Mungu? Je, mtoto hutendewa haki anapolazimishwa kufuata mila na desturi? Je, mtu anaweza kujihesabia haki mbele za Mungu kwa matendo yake mwenyewe? Na ikiwa Ufalme wa Mungu ni haki, je, haki hiyo inaonekana katika maisha yetu ya kila siku?

Maswali haya ndiyo msingi wa toleo hili la RIZIKI. Tunaishi katika ulimwengu “unaolilia haki”, kwa sababu mara nyingi hukutana na upendeleo, dhuluma na mifumo inayomweka mwanadamu mbali na kusudi la Mungu. Mungu hakai kimya. Injili inafunua habari njema kwamba haki ya kweli haianzi katika mahakama za dunia, bali katika kiti cha Mungu kupitia Yesu Kristo.

Toleo hili linaanza mfululizo wa matoleo matatu yanayotafakari Warumi 14:17: “Kwa maana Ufalme wa Mungu si kula na kunywa, bali ni haki, amani na furaha katika Roho Mtakatifu.” Safari inaanza kwa kutazama haki kama msingi wa Ufalme wa Mungu, kabla ya kuendelea na amani na furaha katika Roho Mtakatifu.

Katika kurasa hizi utakutana na ushuhuda wa kupinga mila potofu, mafundisho kuhusu haki ya Kristo, wajibu wa wazazi katika malezi ya watoto, na nafasi ya Mkristo katika kujenga jamii yenye haki.

Tunakualika usisome makala hizi kama maarifa tu, bali kama habari njema inayoaminika kuhusu Kristo Yesu kama haki yetu, na mwaliko wa kuishi maisha ya haki pamoja naye kama Bwana. Hapo ndipo familia hubadilika, jamii hujengwa, na Kristo hutukuzwa.

Next
Next

Tusaidiane kusema ukweli