Twende 1/2026 - Mungu hawezi kuniacha
Cathbert Msemo
Mpendwa Msomaji
Siku moja nilienda sokoni na mama. Kulikuwa na watu wengi, kelele na shughuli nyingi zilizoweza kunichanganya. Ghafla nilipoteza macho kwa muda mfupi. Mara nikahisi nimeachwa peke yangu. Looh! Hofu kubwa ilinijia.
Lakini Mama alikuwa hajaniacha. Mara alinishika mkono na kusema twende huku. Kwa furaha moyo ulitulia, na nilijisikia sijaachwa.
Hivi ndivyo Mungu alivyo pia, hawezi kuniacha nipotee. Yeye ni Baba mwema anayejua mahitaji yangu, na hunishika mkono kila wakati ili nisipotee gizani. Katika maisha hofu inaweza kuja kwa sababu mbalimbali, lakini Mungu yupo siku zote, na anatufariji na kutupa ujasiri na tumaini jipya.
Katika toleo hili utajifunza zaidi juu ya mambo hayo. Kupitia makala nzuri mbalimbali, utaona jinsi ambavyo Mungu hawezi kukuacha upotee. Mungu yupo karibu nawe kila wakati. Furahia pia vibonzo na michezo. Inakufundisha na kukuimarisha kwa namna yake, na ukijibu maswali na kutuma kwetu, utapata zawadi.
Ukiwa na maswali, usisahau kuyatuma kwa Kaka Kalamu. Atakujibu kwa upendo na hekima.
Karibu tusome pamoja toleo hili! Ukiendelea kusoma, ukumbuke kuwa safari ya maisha ni salama na yenye furaha, kwa sababu Mungu hatuachi kamwe.